Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mchango wa wafanyakazi wa kujitolea wapaswa kuthaminiwa zaidi: ripoti

Mchango wa wafanyakazi wa kujitolea wapaswa kuthaminiwa zaidi: ripoti

Wafanyakazi wa kujitolea wana majukumu ya msingi katika kuleta mabadiliko kwenye jamii na kulazimisha serikali kuwajibika kwa raia wao, lakini umuhimu wao hauthaminiwi ipasavyo. Hii ni kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa leo mjini New York kuhusu mpango wa kujitolea wa Umoja wa Mataifa, UNV.

Ripoti hii ni ya kwanza kutathmini mchango wa wafanyakazi wa kujitolea katika maswala ya utawala bora, ikisema ajenda ya maendeleo endelevu itaweza kupata mafanikio iwapo tu itashirikisha jamii zaidi, huku kazi ya kujitolea ikitajwa kama moja ya njia za kushirikisha jamii.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti hii leo mjini New York, Mkuu wa Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa(UNDP), Helen Clark amesema wafanyakazi wa kujitolea wana jukumu la msingi katika kuwakilisha sauti za wale wanaotengwa na uamuzi wa serikali, kama vile wanawake na vikundi vingine.

Takwimu zinaonyesha kuwa serikali zinazowawezesha wafanyakazi wa kujitolea huwa zinanufaika na mchango wao, kwa hiyo ripoti inaomba serikali zingine zichukue hatua ili kusaidia wafanyakazi wa kujitolea kushiriki zaidi katika masuala ya uamuzi wa kisiasa , na pia uundaji wa ajenda za maendeleo.