Skip to main content

ICTR kuhitimisha kazi zake kama ilivyopangwa: Jaji Joensen

ICTR kuhitimisha kazi zake kama ilivyopangwa: Jaji Joensen

Baraza la  usalama la Umoja wa Mataifa leo limejulishwa kuwa ratiba ya kuhitimishwa kwa mahakama ya kimataifa ya uhalifu nchini Rwanda, ICTR iliyoko Arusha nchini Tanzania imesalia kuwa ni ile ile ambayo ni mwishoni mwa mwaka huu.

Hiyo ni kwa mujibu wa Rais wa ICRT, Jaji Vagn Joensen wakati akitoa ripoti ya utekelezaji wa shughuli za baraza hilo mbele ya wajumbe wa Baraza la Usalama jijini New York, Marekani sikuya Jumatano.

Amesema habari njema ni kwamba hadi sasa kesi zote zimekamilishwa isipokuwa moja tu ya Nyimaramasuhuko na wenzake inayohusisha watu Sita ikijulikana zaidi kama rufani ya Butare.

(Sauti  ya Jaji Joensen)

“Hata hivyo hukumu ya rufaa ya kesi ya Butare imepangwa kutolewa baadaye mwaka huu, na kwa uhakika zaidi tunatarajia huku itatolewa katika robo ya nne ya mwaka huu wa 2015. Kufungwa rasmi kwa mahakama hii kunatarajiwa kufanyika kabla ya mwisho wa mwaka huu wa 2015 baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo.”

Wajumbe pia walipata ripoti ya utekelezaji kutoka kwa Theodor Meron ambaye ni Rais wa mahakama ya kimataifa ya  uhalifu wa makosa yaliyofanyika kwa iliyokuwa Yugoslavia, ICTY.

Katika ripoti yake amesema utekelezaji wa majukumu ya chombo hicho ikiwemo kutoa hukumu unakumbwa na changamoto mbali mbali ikiwemo kudorora kwa afya za watuhumiwa na kubainika kwa ushahidi mpya akitolea mfano..

(Sauti ya Jaji Theodor)

Hasa usikilizaji wa kesi dhidi ya Goran Hadžić [HADICH]  imesitishwa kwa muda kutokana na sababu za afya yake. Halikadhalika vikao vya kusikiliza kesi dhidi ya Ratko Mladić, [Mladic] vimepunguzwa hadi vikao vinne kwa wiki kutokana an ushauri wa kimatibabu, na jadala la mashtaka limefunguliwa upya baada ya kupatikana kwa ushahidi mpya.”

Hata hivyo amesema licha ya changamoto hizo, ICTY imeweza kutoa hukumu kwa kesi mbili za rufaa lakini amesema watahakikisha wanaongeza kasi kuhitimisha kama ilivyokubalika.