Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu mpya wa OCHA aapishwa, ni Stephen O’Brien kutoka Uingereza

Mkuu mpya wa OCHA aapishwa, ni Stephen O’Brien kutoka Uingereza

Stephen O’Brien leo ameapishwa rasmi kuwa Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwenye usaidizi wa kibinadamu, akichukua nafasi ya Valerie Amos aliyemaliza muda wake.

Akizungumza baada ya kuapishwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon jijini New York, Marekani, O’Brien amesema ana matumaini makubwa kufanya kazi kwa bidii kwa ushirikiano na jamii ya kimataia wakati huu ambapo watu wengi wana mahitaji na majanga mengi yanahitaji hatua za haraka.

Mratibu Mkuu huyo mpya ambaye pia atakuwa mkuu wa ofisi ya misaada ya kibinadamu, OCHA amewahi kushika nyadhifa mbali mbali ikiwemo mbunge nchini Uingereza na mjumbe maalum wa Waziri Mkuu wa Uingereza kwenye ukanda wa Sahel kati ya mwaka 2012 hadi mwaka huu.

Katibu Mkuu kwa upande wake amemshukuru Bi. Amos kwa utendaji wake wa kujitolea kwa dhati kusaidia watu walio kwenye majanga na mapigano duniani  kote.