Tusongeshe mbele jukumu la walinda amani kila uchao: Ban

29 Mei 2015

Siku ya walinda amani duniani imeadhimishwa maeneo mbali mbali duniani ambapo katika makao makuu ya Umoja huo mjini New York, shughuli hiyo imeongozwa na Katibu Mkuu Ban Ki-moon akisema vitisho vinavyokumba walinda amani hao havitakwamisha azma ya chombo hicho kuendelea kupigania na kulinda amani. Taarifa zaidi na Assumpta Massoi.

(Taarifa ya Assumpta)

Bigula ishara ya kuenzi askari waliopoteza maisha likipulizwa kwenye bustani maalum ya kuenzi walinda amani iliyopo makao makuu ya Umoja wa Mataifa….Hapa ni baada ya Katibu Mkuu kuweka shada kukumbuka walinda amani 126 waliopoteza maisha mwaka jana pekee.

Na ndipo Ban akazungumza akisema hali inazidi kuwa mbaya kila uchao mwaka huu pekee wakiuawa walinda amani 49 kwa hiyo…

(Sauti ya Ban)

“Nachukulia vitisho hivi kwa  umakini wa juu. Tunahitaji uwezo mpya. Hatuwezi kulinda amani karne ya 21 kwa kutumia vifaa vya karne ya 20. Wataalamu wetu wanachukua hatua kuimarisha ulinzi na usalama. Hatuwezi kumaliza vitisho kabisa lakini jamii ya ulinzi wa amani lazima iazimie upya kuwalinda watendaji wetu mizozoni.”

Naye Mkuu wa Operesheni za Ulinzi wa Amani katika Umoja wa Mataifa, Hervé Ladsous,  amesema ili ulinzi wa amani uendelee kukabili ipasavyo mizozo ya sasa na ijayo, unahitaji kuungwa mkono kwa ubia wa kimataifa na utashi wa wote kusaidiana kuubeba mzigo na hatari.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter