Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tujitahidi zaidi kunusuru Libya: Bensouda

Tujitahidi zaidi kunusuru Libya: Bensouda

Mwendesha mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya uhalifu, ICC, Fatou Bensouda, leo amelihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hali inayoendelea Libya, akisema kwamba kuzidi kuzorota kwa hali ya usalama kunaitia wasiwasi siyo tu ICC, bali pia wanachama wa baraza la usalama na jamii ya kimataifa kwa ujumla.

Akitaja mauaji ya raia, mashambulizi ya kigaidi, vitisho dhidi ya waandishi wa habari na wanaharakati wa haki za binadamu, hasa wanawake, amesema jamii ya kimataifa inapaswa kuisaidia Libya ili kuhakikisha uwepo wa uwajibikaji kuhusu mauaji yanayokiuka masharti ya mkataba wa Roma.

Bi Bensouda amependekeza kuwa nchi moja mwanachama yenye uzoefu wa maswala ya sheria wakati wa mpito ijitolee ili kuunda jopo la kimataifa la kuisaidia Libya wakati huu mgumu.

Aidha, licha ya ushirikiano mzuri baina ya ICC na mwendesha mashtaka wa Libya, Bi Bensouda amesikitishwa na baadhi ya vitendo vya serikali ya Libya ambavyo amesema ni kinyume na agizo la ICC, ikiwemo kukataa kumsalimisha Saif Al-Islam Gaddafi kwa ICC.

Hatimaye, amekariri msimamo wake:

(Sauti ya Bensouda)

“ Sisi sote tunaweza na tunapaswa kujitahidi zaidi ili kuhakikisha kuwepo kwa amani na haki nchini Libya. Nitajitahidi kwa upande wangu kusitisha ukwepaji wa sheria, na natarajia kushirikiana na wadau wetu Libya, kupitia jamii, viongozi wa jamii, Umoja wa Mataifa, wanachama wa Mkataba wa Roma, na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya, ili mipango hii izae matunda”