Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNMISS yalaani ghasia kwenye maeneo yanayolindwa Juba:

UNMISS yalaani ghasia kwenye maeneo yanayolindwa Juba:

Barani Afrika, Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS umelaani vikali mapigano yaliyozuka miongoni mwa wakimbizi wa ndani mwishoni mwa wiki katika maeneo inayoyalinda ya raia mjini Juba.

Mtu mmoja aliuawa wakati wa ghasia hizo siku ya Jumapili na wengine takribani 60 walijeruhiwa , hali iliyosababisha wakimbizi wengine wa ndani 35000 kuondoka katika maeneo hayo yanayolindwa.

Mzozo wa ndani unaonekana kuwa chanzo cha mapigano hayo yaliyoanza wiki iliyopita. Toby Lanzer ni naibu mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini na anaelezea hali ilivyo sasa.

(Sauti ya Toby)

"Kuna watu 3,00,000 au zaidi ambao wataachwa bila misada ya uokozi kwa kuwa mashirika ya misaada yameondoka, hii inamaana kama una mtoto anaumwa hakuna mtu katika kituo cha afya kutoa huduma,kama, mtu anahitaji msaada wa chakula hakuna tena huduma."

Awali mvutano ulihusisha wakimbizi wa ndani 350 kutoka jimbo la Unity vitongoji vya Mayom na Mayendit waliokuwa wamejihami kwa mapanga, fimbo na vyuma.

Wanajeshi wa UNMISS na polisi wa kulinda Amani waliingilia na kufanikiwa kutuliza hali lakini mapigano yakazuka Jumamosi Mei 9 katika maeneo matatu. UNMISS ilijitahidi kutuliza hali hiyo lakini mapigano yakazuka tena kwa mara nyingine Jumapili May 10 na kuhusisha wakimbizi wa ndani 400.