Skip to main content

Majibu ya kiafrika kwa matatizo ya kiafrika: rais Museveni aeleza UM

Majibu ya kiafrika kwa matatizo ya kiafrika: rais Museveni aeleza UM

Rais Yoweri Museveni wa Uganda amezungumza katika mjadala wa ngazi ya juu kuhusu ushirikiano baina ya Umoja wa Mataifa na Mashirika ya kikanda uliofanyika leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataida mjini New York na kusema changamoto za Afrika zitatuliwe na viongozi wa Afrika. Taarifa zaidi na Priscilla Lecomte.

(Taarifa ya Priscilla)

Katika mkutano huo wa ngazi ya juu, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amezingatia umuhimu wa mashirika ya kimataifa katika kukuza maendeleo endelevu na amani ya kimataifa kwenye kanda zao na haja ya kuimarisha uhusiano kati yao na Umoja wa Mataifa.

Ameongeza kwamba changamoto zinazokumba dunia ya sasa zinalazimu kutegemea zaidi mashirika ya kikanda.

“ Jamii ya kimataifa inapaswa kuhudumia wanachama wanaohitaji zaidi lakini mara nyingi tunashindwa. Mashirika ya kimataifa yameshaimarisha ufanisi wetu. Lakini sasa tunapaswa kufanya zaidi ili kujibu vilio vya mamilioni ya watu wanaostahili utu kamili na usawa wa ukweli.”

Naye Rais wa Uganda Yoweri Museveni amesisitiza umuhimu wa kusikiliza sauti za mashirika ya kikanda katika maswala ya amani ya kimataifa, akiongeza kwamba ni lazima kubadilisha mfumo wa Umoja wa Mataifa hasa Baraza la Usalama.

“ Majibu ya kiafrika kwa matatizo ya kiafrika. Jamii ya kimataifa ikiwemo Umoja wa Mataifa inapaswa kuheshimu utaratibu za kikanda. Hii ndiyo itatusaidia kuzuia Umoja wa Mataifa utumiwe kwa faida za kitaifa au vikundi vya wanachama wenye nguvu na kudhoofisha juhudi za mashirika ya kikanda na amani duniani”