Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Matumizi endelevu ya misitu ni muhimu kwa ajili ya kutokomeza umaskini

Matumizi endelevu ya misitu ni muhimu kwa ajili ya kutokomeza umaskini

Wakati wa uzinduzi wa kongamano la Umoja wa Mataifa kuhusu misitu, lililoanza leo mjini New York, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Jan Eliasson ametoa wito wa matumizi endelevu ya misitu ambayo inatoa riziki kwa watu bilioni 1.6 duniani kote.

Wakati washiriki wa kongamano hilo la wiki mbili wanatarajiwa kufikia makubaliano ya kimataifa kuhusu misitu, bwana Eliasson amesema yatakuwa ni ya msingi katika kutimiza malengo ya maendeleo endelevu ya baada ya mwaka 2015.

« Makubaliano ya kimataifa kuhusu misitu yenye nguvu zaidi yatatoa mwongozo ambao utawezesha kukabiliana na changomoto hizo, ili rasilimali za misitu duniani kote ziweze kukidhi mahitaji ya watu, leo na katika siku za usoni. »

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, matumizi endelevu ya misitu ni mfumo wenye ufanisi zaidi wa kuhifadhi gesi chafuzi duniani.

Aidha Naibu Katibu Mkuu amezingatia maswala ya utawala bora katika kupambana na matumizi haramu ya misitu na uharibifu wake, na pia ushiriki zaidi wa jamii na hasa jamii asilia ambazo zina ujuzi zaidi kuhusu misitu.