Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNFPA yaimarisha usaidizi kwa walionasuliwa kutoka Boko Haram

UNFPA yaimarisha usaidizi kwa walionasuliwa kutoka Boko Haram

Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu, UNFPA Dkt. Babatunde Osotimehin amezungumzia hatua ambazo shirika lake linachukua kufuatia tukio la hivi karibuni la kuokolewa kwa wanawake na watoto wa kike kutoka kikundi cha kigaidi cha Boko Haram nchini Nigeria.

Akizungumza na waandishi wa habari nchini humo, ametaja hatua hizo kuwa ni pamoja na kuhakikisha watoto wa kike wanarejea shuleni sambamba na huduma ya usaidizi wa kisaikolojia kwa kuwa athari za kifikra walizopata ni kubwa kuliko ilivyodhaniwa..

(Sauti ya Babatunde)

“Ushauri nasaha unapaswa kuwa wa kina zaidi, kuzungumza nao mmoja mmoja na kuhakikisha wanajisikia vizuri ni jambo zuri. Nafurahi kwamba jamii haiwatengi, imewakubali  na naamini hiyo ni aina nzuri sana ya tiba kuweza kufanya hivyo.”

Dkt. Babatunde amesema UNFPA iliwapatia mafunzo ya utoaji ushauri nasaha wanajamii 60 ambao ndio wanatekeleza jukumu hilo kwa wanawake na watoto hao wa kike.