Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR kupunguza madhila katika vituo vya uhamiaji Libya:

UNHCR kupunguza madhila katika vituo vya uhamiaji Libya:

Nchini Libya shirika la Umoja wa mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limekuwa likisaidia watu wapatao 1,242 waliookolewa baharini na walinzi wa Pwani wa Libya , kutokana na safari zisizo salama za boti karibu na Tripoli katika siku 10 zilizopita, ambao wengi wamepelekwa kwenye vituo vya uhamiaji.

Idadi hii inajumuisha kundi la watu zaidi ya 200 kutoka pembe ya Afrika ambapo wane kati yao wameungua vibaya kutokana na mlipuko wa gesi wiki mbili zilizopita katika eneo lisilojulikana walikokuwa wanashikiliwa na wasafirishaji kinyemela wa watu kabla ya kuanza safari ya boti kuelekea Ulaya.

UNHCR imesema ina taarifa ya takribani wahamiaji au waomba hifadhi 2,663 wakiwemo wanawake na watoto ambao wako katika vituo vinane vya uhamiaji nchini Libya vinavyoendeshwa na idara ya kukabiliana na wahamiaji haramu nchini humo.

Wengi wa watu katika vituo hivyo ni raia wa Eritrea, Ethiopia, raia wa Sudan na kutoka nchi mbalimbali za Afrika ya Magharibi.