Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Takwimu za matumizi ya simu na uokoaji wa maisha na kutokomeza njaa:WFP

Takwimu za matumizi ya simu na uokoaji wa maisha na kutokomeza njaa:WFP

Shirika la mpango wa chakula duniani, WFP kwa ushirikiano na Global Pulse iliyobuniwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya takwimu, wameshirikiana kuona jinsi gani takwimu za matumizi ya simu za mkononi zinaweza kusaidia harakati za kukabiliana na njaa na kuokoa maisha. Taarifa zaidi na Grace Kaneiya.

(Taarifa ya Grace)

WFP na Global Pulse wamekuwa na miradi ya utafiti inayochambua uhusiano kati ya matumizi ya simu za mkononi na njaa ambapo matokeo yake yatawasilishwa wiki hii kwenye mkutano utakaofanyika katika taasisi ya teknolojia ya  Massachussetts nchini Marekani.

Mchumi mkuu wa WFP Arif Husain amesema mwelekeo huo ni mbinu mpya ya kutoa usaidizi wa kibinadamu kwa kuwa kadri mashirika yanaridhia mbinu mpya, ukusanyaji taarifa utakuwa rahisi na wa haraka na hivyo kurahisisha pia upelekaji wa mahitaji kwa watu wenye njaa duniani.

Miradi imejikita kwenye jinsi takwimu za matumizi ya simu za mkononi zinaweza kuchambuliwa na kuelewa mwelekeo wa njaa katika kaya na jinsi inaweza kuwa hatarini kukumbwa na majanga.

Mathalani kukadiria matumizi ya kaya kwenye mlo barani Afrika na mbinu ya kubaini kaya zinazojitaji msaada huko Mexico.

Hata hivyo taasisi hizo mbili zimeomba kampuni za simu za mkononi kutoa  ushirikiano katika utoaji wa takwimu hizo huku msisitizo ukiwekwa kwenye kuzingatia faragha za watumiaji.