Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Raia Yemen na Syria wanateseka, mapigano yasitishwe hima: Ban

Raia Yemen na Syria wanateseka, mapigano yasitishwe hima: Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki- Moon ametaka kupatikana hima kwa suluhu la mzozo baina ya serikali na waasi nchini Yemen ili kuwaepusha raia katika dhiki wanayopata kufuatia kuendelea kwa mzozo huo.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini New York , Bwana Ban amesisitiza kuwa majadiliano ndiyo muarobaini wa kumaliza tofauti za pande kinzani na kuangazia kile raia wanachokabiliana nacho.

(SAUTI BAN)

Familia nchini Yemen zinateseka katika mahitaji muhimu kama vile maji, chakula mafuta na madawa. Mamia ya raia wameuwawa .Hospitali na shule zinafungwa, baadhi yao zinalengwa moja kwa moja katika mapigano

Amerejelea kauli yake kuwa kitendo cha waasi wa Houthi na washirika wao kutaka kuchuku dola kwa nguvu na kuidharau serikali halali ni uvunjaji wa wazi wa maazimio ya baraza la usalama na hadio zao katika mchakato wa kisiasa wa upatanishi unaoendelea chini ya uratibu wa Umoja wa Mataifa.

Kuhusu Syria Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema sasa uhalifu na machafuko yanayoendelea ni ya kupindukia akitolea mfano wa kambi ya Yarmouk ambayo ameiita ni kisiwa cha kuzimu akisema wakimbizi 18000 wa Palestina na Syria sasa wanashikiliwa mateka na kundi la kigaidi linalotaka dola ya kiislamu , Daesh au ISIS.

Bwana Ban amesema kambi hiyo inaelekea kufanana na kambi ya kifo akitolea mfano wa watoto 3500 waliogeuzwa ngao ya binadamu katika mapigano hivyo akatangaza hatua ya dharura.

(SAUTI BAN)

Tunachohitaji kufanya haraka ni kuweka utulivu kambini. Naungana na baraza la usalama katika kutaka usitishwaji wa uhasama , ufikishwaji wa misaada ya kibinadamu na kuondolewa salama kwa raia ambao wanataka kuondoka katika eneo hilo.

Ametaka nchi wanachama zenye ushawishi kwa serikali na pande kinzani kuchukua hatua zote muhimu kutuma ujumbe kuwa raia lazima walindwe wakati wote.

Katibu Mkuu Ban anaondoka hii leo kuelekea Panama kuhudhuria mkutano kuhusu sera za mataifa ya Amerika kabla ya kwenda Doha, Qatar kuhudhuria mkutano kuhusu kuzuia uhalifu.