Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ripoti ya tathmini ya elimu kwa wote 2000-2015 yazinduliwa

Ripoti ya tathmini ya elimu kwa wote 2000-2015 yazinduliwa

Katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa kumefanyika uzinduzi wa kimataifa wa ripoti ya ufuatiliaji wa elimu duniani mwaka 2000-2015, mafanikio na changamoto inayoeleza pamoja na mambo mengine kuwa dola Bilioni 22 za nyongeza zinahitajika ili kusaidia mataifa duniani kufikia malengo ya elimu kwa wote ifikapo mwaka 2030.

Akizungumza kwenye  uzinduzi wa ripoti hiyo ambayo ni toleo la 12, Mkurugenzi wa shirika la elimu, sayansi na utamaduni, UNESCO, ofisi ya New York, Bi. Moufida Goucha amesema utashi wa kisiasa umewezesha serikali kuwekeza kwenye elimu kwa wote licha ya kutofikiwa kwa ukamilifu malengo yote yaliyowekwa miaka 15 iliyopita huko Senegal.

Mathalani licha ya kuongezeka kwa uandikishaji, bado uwiano wa uandikishaji ni changamoto, huku zaidi ya theluthi moja ya watoto wasio shuleni wakiwa ni wale walioko kwenye maeneo ya mizozo, hivyo akasema..

(Sauti ya Bi. Goucha)

Tunavyokaribia ukomo wa majadiliano kuhusu malengo ya maendeleo endelevu baada ya mwaka 2015, tuna uhakika kuwa ajenda hiyo itatoa hakikisho la elimue na fursa za kujifunza kwa wote.”

Kwa mujibu wa ripoti hiyo Theluthi mbili ya wajinga wa kutokujua kusoma na kuandika duniani ni wanawake ambapo kwa nchi za Afrika zilizo Kusini mwa jangwa la Sahara, nusu ya wanawake hawana kabisa stadi za kuondoa ujinga.