Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Twasikitishwa na hukumu ya kifo Gambia: Zeid

Twasikitishwa na hukumu ya kifo Gambia: Zeid

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu kwenye Umoja wa Mataifa Zeid Ra’ad Al Hussein amesikitishwa na hukumu ya kifo iliyotangazwa wiki iliyopita na mahakama ya kijeshi nchini Gambia dhidi ya watuhumiwa watatu wa jaribio la mapinduzi ya kijeshi nchini humo.

Watuhumiwa hao wanadaiwa kutenda kosa hilo mwezi Disemba mwaka jana ambapo wengine watatu wamehukumiwa adhabu ya kifungo cha maisha na mahakama hiyo hiyo ambayo kwa mujibu wa Kamishna Zeid mchakato wa mzima wa kesi ulikuwa wa siri.

Taarifa ya ofisi ya haki za binadamu imemkariri Kamishna Zeid akisema kuwa uendeshaji huo wa kesi ni kinyume na vipengele vya katiba na sheria ya majeshi ya ulinzi ya Gambia ambavyo vinataka kesi zote zisikilizwe hadharani.

Amesema hofu pia inatokana na haki katika mchakato mzima wa kesi hususan suala la uwakilishi wa kisheria kwa watuhumiwa hao ambao ni  haki yao kisheria.

Kamishna huyo wa haki za binadamu amesema ni matumaini yake kuwa watuhumiwa wote sita ambao bado wanashikiliwa wataruhusiwa kukata rufaa kwa kuwa ni haki yao ya msingi.

Halikadhalika ametoa wito kwa serikali ya Gambia kuendeleza sitisho lake la matumizi ya adhabu ya kifo.