Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vijidudu kwenye chakula vyaua watu 351,000: WHO

Vijidudu kwenye chakula vyaua watu 351,000: WHO

Shirika la afya duniani, WHO limetaka usimamizi thabiti wa hatua za usalama wa chakula ili kuepusha maambukizi ya magonjwa kwani mwaka 2010 pekee watu zaidi ya Laki Tatu na Nusu walifariki dunia kwa sababu ya magonjwa yatokanayo na vijidudu na vimelea kwenye chakula.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi kuhusu mada ya usalama wa chakula ambayo ndiyo maudhui ya siku ya afya duniani mwaka huu, Mkurugenzi wa Usalama wa chakula WHO Kazuaki Miyagishima amesema usalama wa chakula uko hatarini zaidi wakati huu ambapo utandawazi unahusisha maeneo mbali mbali kuzalisha, kufungasha na kusafirisha chakula akisema ni jambo zuri kimaendeleo lakini usalama uzingatiwe.

(Sauti ya Miyagishima)

“Viambato au vyakula vibichi husafirishwa maelfu ya kilometa hadi nchi nyingine ambako hufanyiwa matayarisho mengine na kufungashwa. Halafu kusafirishwa hadi nchi nyingine ambako hutengenezwa na kuwa chakula kamili na kusambazwa kwenye nchi nyingine. Hii ina maana mlolongo mzima wa kupata chakula umekuwa mrefu sana.”

Mkurugenzi huyo akasema barani Ulaya angalau serikali zimeweka mamlaka moja lakini kwenye nchi nyingine hakuna uratibu wa jambo hilo ambalo ni mtambuka.

(Sauti ya Miyagishima)

“Kwenye nchi nyingine nyingi, usalama wa chakula ni wajibu wa vyombo vingi na mara nyingi havina mawasiliano, kwa hiyo kuna hatari nyingi zinazoweza kusababishwa na vile ambavyo ambavyo serikali zinashughulikia suala hilo.”

Vijidudu na vimelea vinavyotajwa kuleta madhara ya afya kwa binadamu kutokana na maandalizi hafifu ya chakula kuanzia shambani hadi kinapomfikia mlaji ni pamoja na Salmonella na E.coli.