Kinga na hadhi ya watendaji wa UM viheshimiwe: Ban

25 Machi 2015

Katika siku ya kuonyesha mshikamano na wafanyakazi wanaoshikiliwa au wasiojulikana waliko, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ametaka kuimarishwa kwa juhudi za kulinda watendaji hao wanapokuwa kwenye majukumu yao.

Ban amesema ghasia na mizozo iliyoenea mwaka uliopita imekuwa na gharama kwa Umoja wa Mataifa na watendaji wake kwani hadi tarehe 15 mwezi huu wafanyakazi 33 wanashikiliwa na serikali kwenye nchi 15.

Amesema kama hiyo haitoshi mfanyakazi mmoja hajulikani aliko huku makandarasi wawili wakiwa wanashikiliwa kizuizini na waliowateka nyara.

Ban ametumia ujumbe wake wa siku hii kusihi serikali kuheshimu hadhi na kinga walizonazo wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na washirika wao ambao bado wanashikiliwa kinyume cha sheria.

Halikadhalika amesihi vikundi vilivyojihami ambavyo si vya kiserikali na ambavyo vinashikilia watendaji hao kuwaachia huru mara moja.

Katibu Mkuu amesema usalama wa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na washirika wao ni lazima liwe jukumu la pamoja linalopatiwa kipaumbele na pande zote husika.

Baadhi ya maeneo ambako wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wamekumbwa na zahma ni pamoja na Afghanistan, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Sudan.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter