Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Licha ya mafanikio Kifua Kikuu bado ni tishio tuchukue hatua:WHO

Licha ya mafanikio Kifua Kikuu bado ni tishio tuchukue hatua:WHO

Leo ni siku ya Kifua Kikuu, TB, duniani ambapo shirika la afya duniani, WHO linataka utekelezaji wa mkakati wenye lengo la kuwa na dunia isiyo na vifo vitokanavyo na Kifua Kikuu, wagonjwa sambamba na machungu yatokanayo na ugonjwa huo ili kuendeleza mafanikio yaliyopatikana kupitia utambuzi mapema wa wagonjwa.

Mkakati huo unataja misingi mikuu mitatu ya kuzingatiwa na wadau wakuu kwenye mpango huo ambao ni serikali, wadau wa kimataifa, mashirika yasiyo ya kiserikali na jamii.

Misingi hiyo ni mosi,  wagonjwa kuwa kitovu cha huduma, pili sera thabiti, na tatu tafiti na mbinu bunifu ili kukabiliana na ugonjwa huo.

Mathalani msingi wa kwanza unataka kila mgonjwa kupata huduma bila ubaguzi wakati huu ambapo WHO inasema wagonjwa Milioni Tatu hawapati huduma na hivyo kuwa moja ya sababu ya kuendelea kuwepo kwa Kifua Kikuu sugu.

Katika ujumbe wake wa siku hii, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema sasa ni fursa ya kutokomeza Kifua Kikuu ifikapo mwaka 2035 ili kumaliza machungu kwa familia zinazokabiliwa na ugonjwa huo.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt.Margaret Chan ametaka mshikamano wa dunia kuondokana na kifua kikuu wakati huu ambapo WHO inasema kuna pengo la dola Bilioni Mbili kila mwaka katika shughuli za tafiti dhidi ya Kifua Kikuu.