Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Machafuko Nigeria yamesababisha tatizo kubwa la kibinadamu- OCHA

Machafuko Nigeria yamesababisha tatizo kubwa la kibinadamu- OCHA

Mzozo kaskazini mashariki mwa Nigeria umekuwa na athari kubwa, zikiwemo kuchangia idadi kubwa ya kukimbia makwao, ukiukwaji mkubwa wa sheria ya kimataifa ya kibinadamu, sheria ya haki za binadamu na kuongezeka kwa tatizo la kibinadamu. Hayo yamesemwa na Mkuu wa Operesheni za Kibinadamu katika Ofisi ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu, OCHA, John Ging, ambaye amehitimisha ziara yake nchini humo hivi karibuni, aliyoifanya na maafisa wengine 11 wa ngazi ya juu kutoka mashirika ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa na wadau wengine.

Akihutubia waandishi wa habari mjini New York, afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amesema zaidi ya watu milioni moja wamelazimika kuhama makwao ndani ya nchi, huku wengine wapatao 200,000 wakiwa wamekimbilia nchi jirani, hususan Cameroon, Chad na Niger.

“Inakadiriwa kuwa zaidi ya raia 6,300 wameuawa katika mapigano kufikia sasa, na maelfu yaw engine wameripotiwa kupata majeraha mabaya sana na maafa mengine, hususan ukatili dhidi ya wanawake na watoto. Zaidi ya shule 300 zimefungwa, na Nigeria pia inakabiliana na na mlipuko wa kipindupindu, surua na meningitis. Kuna uhaba wa maji na huduma za kujisafi, na kuongezeka kwa utapia mlo kunatia wasiwasi.”

Ging amesema asilimia 90 ya watu waliofurushwa makwao wanaishi katika makazi duni na wengine wanapewa makazi na jamii walikokimbilia.

“Hilo linaweka mzigo mkubwa jamii za wenyeji wao kukimu. Tulienda kujionea hali Yola. Mji huo, kabla ya mzozo, ulikuwa na takriban watu 300,000, lakini sasa, idadi hiyo imeongezeka maradufu, kwani sasa una wakimbizi wa ndani zaidi ya 300,000 waliotafuta makazi katika mji huo. Hilo linaibua changamoto kubwa kwa kila mtu, na hususan jamii ya wenyeji wao.”

Amesema athari za kikanda za mzozo huo pia zinaongezeka, akiongeza kwamba athari za muda mrefu zitakuwa mbaya hata zaidi, kwani eneo la Sahel hutegemea sana chakula kinachozalishwa Nigeria, na sasa uzalishaji wa kilimo umeathiriwa vibaya mno na machafuko.