Hatua za kuondoa MONUSCO DRC zizingatie taratibu maalum: Kobler
Wakati baraza la usalama likielekea kuongeza muda wa ujumbe wake huko jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC MONUSCO kwa mwaka mmoja zaidi, imeelezwa kuwa mpango wowote wa kuhitimisha shughuli za ujumbe huo ni lazima uzingatie taratibu maalum ili kuhakikisha nchi inabakia salama kwa mustakbali wa taifa zima. Ripoti ya Assumpta Massoi inafafanua zaidi.
(Taarifa ya Assumpta)
Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa huko DRC Martin Kobler amesema hayo katika hotuba yake kwa baraza siku ya Jumanne ikigusia masuala manne, uchaguzi ujao, hali ya usalama, harakati za kuleta utulivu DRC na kurejesha kuaminiana kati ya Umoja huo na serikali.
Kobler akasema miaka 15 MONUC ikiingia DRC nchi ilikuwa vitani lakini sasa angalau imeungana kwa kiasi fulani lakini bado kuna mambo ya kufanya ili kuwepo na amani endelevu. Hivyo akasema MONUSCO haitakuwepo maisha nchini humo, wakati itafika itaondoka lakini..
(Sauti ya Kobler)
“Hatua zaidi zinahitajika kupunguza vitisho na ghasia dhidi ya raia kutoka vikundi vilivyojihami na hatua hizo ziwe za kiwango ambacho zinafanywa na taasisi za umma zinazowajibika. Halikadhalika kufikia utulivu kwa kuanzisha taasisi za umma zinazofanya kazi na kuzingatia weledina. Pia kuweka taratibu za kidemokrasia.”
Mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa UM kwa nchi za maziwa makuu Said Djinnit akawasilisha ripoti ya katibu mkuu kuhusu utekelezaji wa mkataba wa amani kwenye ukanda huo akisema miaka miwili tangu usainiwe, ukanda huo uko njia panda kwani utekelezaji unasuasua.