Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza lalaani shambulio la kigaidi Tunisia

Baraza lalaani shambulio la kigaidi Tunisia

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wamelaani vikali shambulio la kigaidi yaliyofanywa kwenye makumbusho ya kimataifa mjini Tunis, Tunisia siku ya Jumatano na kusababisha vifo vya watu wapatao 20.

Katika taarifa yao wajumbe hao wametuma rambirambi zao kwa familia za wahanga na serikali ya Tunisia huku wakisisitiza umuhimu wa watuhumiwa wa shambulio la kikatili halikadhalika waliopanga na waliofadhili wakamatwe na wafikishwe mbele ya sheria.

Halikadhalika wameziomba nchi zota kwa mujibu wa sheria za kimataifa na maazimio mengine husika ya baraza la usalama washikamane na wasaidie Tunisia kwenye harakati hizo.

Wajumbe hao wamesema hakuna shambulio lolote linaloweza kubadili mwelekeo wa demokrasia, ukwamuaji wa kiuchumi na maendeleo nchini Tunisia.

Kwa mantiki hiyo wamesisitiza umuhimu wa kukabiliana na vitisho vyote vya amani na usalama kwa njia zote zinazozingatia misingi ya Umoja wa Mataifa.

Wamesisitiza kuwa hakuna shambulio lolote lile la kigaidi au uhalifu unaoweza kuhalalishwa kwa misingi yoyote ile.