Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wito mpya kwa Haiti watolewa na OCHA

Wito mpya kwa Haiti watolewa na OCHA

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuratibu Misaada ya Kibinadamu, OCHA, limetoa wito mpya wa ufadhili kwa ajili ya Haiti, miaka mitano baada ya tetemeko la ardhi lililokumba kisiwa hiki na kusababisha vifo zaidi ya 200,000.

Msaidizi wa Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu nchini humo Peter de Clercq amesema ni wito wa aina mpya kwani unalenga kutafuta suluhu endelevu kwa matatizo ya Haiti.

“ Hatuwezi kuendelea kutoa misaada ya kibinadamu kwa matatizo ambayo ni ya kimaendeleo na ya muda mrefu. Nilipotemebelea maeneo yaliyokumbwa na mafuriko nchini Haiti mwaka huu, nimeambiwa kwamba maeneo hayo yanafurika kila mwaka, na huenda yatafurika tena mwaka kesho. Sasa kuliko kuja kila mwaka na msaada wa kibinadamu kwanini tusiangalie uwezekano wa serikali wa kuhamishia watu kwenye maeneo ambayo hayatakumbwa na mafuriko kila mwaka?”

Moja ya nguzo za mkakati huo mpya wa dola milioni 400 ni kuhamisha wakimbizi wa ndani ambao idadi yao ni 79,000 na watu wanaoishi kwenye maeneo yanayoweza kufurika mara kwa mara.

Aidha OCHA inatarajia kutokomeza mlipuko wa kipindupindu unaoendelea Haiti na pia kuzuia milipuko mingine isitokee tena kwa kuimarisha mifumo ya maji na maji safi.

Hatimaye, mkakati huo utalenga kuimarisha uwezo wa jamii wa kujitahadhari na majanga kama mafuriko na matetemeko ya ardhi, na kujenga uwezo wa serikali katika maswala haya.