Mfumo wa maendeleo wa Umoja wa Mataifa wahitaji ufanisi na ushirikiano zaidi

Mfumo wa maendeleo wa Umoja wa Mataifa wahitaji ufanisi na ushirikiano zaidi

Licha ya mafanikio katika mfumo wa msaada wa kimaendeleo, Umoja wa Mataifa unahitaji kuimarisha utoaji msaada ili kutokomeza umaskini.

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Jan Eliasson amesema hayo akihutubia mkutano wa Baraza la Uchumi na Kijamii la Umoja wa Mataifa ECOSOC kuhusu shughuli za mfumo wa maendeleo wa Umoja wa Mataifa, uliofanyika mjini New York.

Ametaja ripoti ya Katibu Mkuu kuhusu maswala hayo ikionyesha kwamba Umoja wa Mataifa umejitahidi kuboresha ufanisi wa utoaji misaada ya kimaendeleo, kwa kuheshimu zaidi mipango ya serikali, kutumia taaluma zilizopo kwa ngazi ya kitaifa au kurahisisha mifumo ya ufadhili.

Hata hivyo Eliasson amesema changamoto zipo, serikali na wananchi wakilalamikia ugumu na urasimu wa mfumo wa Umoja wa Mataifa.

Ametaja sehemu zinazoweza kuboreshwa ikiwemo kutumia zaidi teknolojia mpya au kuongeza ushirikiano baina ya mashirika ya Umoja wa Mataifa.

“ Mfumo wa maendeleo ya Umoja wa Mataifa una uwezo mkubwa. Uko kila sehemu duniani, una uzoefu mwingi. Ina maana tuko na uwezo wa kipekee wa kubaliana na changamoto za siku hizi. Tunatarajia kujenga juu ya nguvu zetu. Lakini tunataka kuhakikisha pia kwamba Mfumo wa maendeleo wa Umoja wa Mataifa unafanya kazi kwa mshikamano zaidi ili kutekeleza kama mfumo mmoja. Hatutaki tu kukabiliana na changamoto, tunataka kuzishinda”.

Kwa mujibu wa ripoti ya Katibu Mkuu, asilimia 63 ya matumizi ya Umoja wa Mataifa huelekezwa kwenye shughuli za maendeleo, asilimia 18 ikiwa ni kwa ajili ya ulinzi wa amani, na asilimia 47 ya pesa hizo zikitumiwa kwenye ukanda wa Afrika.

Aidha katika nchi kumi zilizopokea msaada mwingi zaidi mwaka 2013, nchi saba ziko Afrika nazo ni Nigeria, DRC, Zimbabwe, Sudan, Sudan Kusini, Ethiopia na Somalia.