Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ya watu wa Syria inazidi kuzorota pasipo suluhu la kisiasa - Ripoti

Hali ya watu wa Syria inazidi kuzorota pasipo suluhu la kisiasa - Ripoti

Ripoti mpya ya tume ya uchunguzi kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Syria imesisitiza haja ya kuendeleza juhudi za kutafuta suluhu la kisiasa kwa mzozo wa Syria ili kuepusha ukiukaji zaidi wa haki za binadamu. Taarifa kamili na Assumpta Massoi

(Taarifa ya Assumpta)

Ripoti hiyo iliyowasilishwa kwa Baraza la Haki za Binadamu imesema kuwa, mzozo wa Syria ambao ulianza kama maandamano mnamo mwezi Machi mwaka 2011, sasa umebadilika na kujumuisha makundi mengi ambayo hayaheshimu kabisa sheria ya kimataifa.

Huku ikimulika hatua zilizochukuliwa kimataifa na zile ambazo hazijachukuliwa, ripoti hiyo inalenga kusisitiza hali mbaya na mateso yanayowakumba raia wa Syria pasipo suluhu la kisiasa kwa mzozo huo.

Tume hiyo imekariri mapendekezo iliyofanya katika ripoti zake za awali, ikitaka pande husika ziheshimu haki za binadamu, sheria ya kimataifa ya kibinadamu na maazimio ya Baraza la Usalama.

Ripoti imezitaka pande zote zipambane na uenezaji wa ukiukwaji wa haki, misimamo mikali na ugaidi kwa kuwafikisha mbele ya sheria wanaotenda uhalifu huo, huku zikitoa ulinzi na usaidizi kwa raia, wakiwemo wakimbizi.