Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mazungumzo ya amani kuhusu Syria kuendelea Jumapili

Mazungumzo ya amani kuhusu Syria kuendelea Jumapili

Wajumbe wa serikali ya Syria na wale wa upinzani wamekuwa na mazungumzo ya ana kwa ana huko Geneva, Uswisi ikiwa ni mara ya kwanza tangu kuanza kwa mzozo nchini mwao.

Ajenda kuu siku ya Jumamosi kwenye mazungumzo hayo chini ya usuluhishi wa Lakhdar Brahimi mjumbe wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa nchi za kiarabu ilikukwa ni kuwezesha misaada ya kibinadamu kuwafikia walengwa hususan huko Homs ambako maelfu ya raia wamekwama bila misaada.

Bwana Brahimiameaambia waandishi wa habari kuwa ijapokuwa pande hizo hazikuwa na mazungumzo ya moja kwa moja kumekuwepo na maendeleo ambapo kuna msafara wa misaada ya chakula na vifaa vingine muhimu kwenda maeneo husika na amesema anatumai vitaruhusiwa Jumapili.

Mjumbe huyo maalum amesema majadiliano yataendelea kesoh na ajenda itakuwa ni kuachiwa huru kwa watu wanaoshikiliwa na serikali pamoja na upinzani.

Umoja wa mataifa umekuwa unataka kuachiwa huru kwa wanawake, wazee na watoto. Nina matumaini makubwa na majadiliano ya kesho na nasali tuwe na habari njema.

Amesema vita nchini Syria imekuwa fursa ya ugaidi kuota mizizi na kutanuka huku akisema kuwa kumaliza vita ndiyo suluhu ya kuushinda ugaidi.

Tunashughulikia siyo tu ugaidi pekee bali pia masuala yote ya vita na ninatumai ugaidi utapungua kwanza na hatimaye kutokomezwa iwapo vita vitamalizika na amani kurejea Syria.

Bwana Brahimi amesisitiza kuwa tamko la pamoja la Geneva la mwezi Juni mwaka 2012 linabakia kuwa msingi wa mazungumzo ya amani ya Syria.