Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mitandao ya kijamii inaboresha mawasiliano kuhusu diplomasia

Mitandao ya kijamii inaboresha mawasiliano kuhusu diplomasia

Matumizi ya mitandao ya habari ya kijamii kwenye Umoja wa Mataifa yana umuhimu wake kwani inapotumiwa na mabalozi, mitandao hiyo inawawezesha kutoa taarifa kuhusu shughuli za kidiplomasia upesi.

Kauli hiyo imetolewa na watafiti waliochapisha ripoti mpya kuhusu faida za mitandao kama vile Twitter na Facebook katika uhusiano wa kidiplomasia, wakati wa mkutano uliongaziwa suala la mitandao hiyo ya kijamii leo, ikiwa ni Siku ya Mitandao ya Kijamii kwenye Umoja wa Mataifa.

Adam Snyder anayefanya tathmini kwenye kampuni ya kibinafsi ya Burson-Marsteller, amemweleza  Daniel Dickinson wa Redio ya Umoja wa Mataifa kuhusu jinsi wanadiplomasia wanavyotumia Twitter.

Mfano bora ninaoweza kutumia kueleza, ni mabalozi wanavyotumia Twitter kuwafahamisha watu wanaowawakilisha kuhusu kazi wanayoifanya- na hivyo inawawezesha kuwa karibu zaidi, kwa mfano anaweza kusema, nilikutana na balozi fulani, na tulizungumza  kuhusu suala hili na lile, au nalipa kipaumbele suala fulani. Nadhani inachofanya, ni kwamba, imebadilisha mawasiliano ya diplomasia kuwa ya papo hapo. Miaka 10 iliyopita, ili balozi aeleze kuwa amekuwa kwenye mkutano na wamejadilia suala fulani, ilibidi aandike barua au taarifa kwa vyombo vya habari, lakini sasa inafanyika papo hapo”