Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukatili Syria umezidi kiwango hata tunaishiwa maneno: Amos

Mkuu wa OCHA, Bi. Valerie Amos (Picha:Valerie Amos. UN/Kim Haughton)

Ukatili Syria umezidi kiwango hata tunaishiwa maneno: Amos

Mkuu wa masuala ya uratibu wa misaada ya kibinadamu kwenye Umoja wa Mataifa Valerie Amos amelihubutia Baraza la usalama akisema kiwango cha ukatili dhidi ya raia huko nchini Syria kimefikia kiwango ambacho hata wanakosa maneno ya kuelezea.

Amesema ukatili huo unafanyika licha ya Baraza la usalama mwezi Februari mwaka huu kupitisha azimio namba 2139 ambalo pamoja na mambo mengine lilitaka pande zote kwenye mzozo kuhakikisha ulinzi kwa raia walionaswa kwenye maeneo ya mapigano na kuzingatia haki za kibinadamu za kimataifa.

(Sauti ya Amos)

“Kila wakati tunapotoa takwimu mpya kuhusiana na mzozo wa Syria tunasema ni kiwango kisichokuwa cha kawaida. Tumeishiwa maneno ya kuelezea kwa kina ukatili, ghasia na dharau ya uhai wa binadamu ambayo ndiyo alama ya mzozo huu. Jamii ya kimataifa imekumbwa na ganzi kutokana na athari ya idadi kubwa, kusambaa kwa mzozo na mkwamo wa kisiasa.”

Bi Amos ambaye pia ni mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoratibu misaada ya kibinadamu amesema hata kwenye vita kuna kanuni kwani kumnyima mtu matibabu kama silaha ya vita haikubaliki kisheria.

Pamoja na kurejea ombi lake la kutaka Baraza la Usalama lihakikishe pande husika zinazingatia azimio namba 2139, Bi. Amos amesema jambo muhimu zaidi ni..

(sauti ya Amos)

 "Baraza hili na jamii ya kimataifa lazima wasake suluhu ya kisiasa ili kumaliza kabisa mzozo huu.”