Waliouawa Beni wafikia 200, Baraza la usalama lalaani

26 Novemba 2014

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wamelaani vikali mauaji dhidi ya raia yaliyofanyika tarehe 20 mwezi huu huko Beni, jimbo la Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Mashambulio hayo yameongeza idadi ya raia waliouawa tangu ghasia zianze kwenye eneo hilo katikati ya mwezi uliopita kufikia 200.

Wajumbe katika taarifa yao pamoja na kutuma rambirambi kwa wafiwa wamelaani pia mashambulizi dhidi ya walinda amani wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, MONUSCO wakisema jaribio lolote la kukandamiza uwezo wa ujumbe huo hautavumiliwa na wametaka wahusika wafikishwe mbele ya sheria.

Halikadhalika wamerejelea msimamo wao wa kuunga mkono MONUSCO na kutaka pande zote kushirikiana ili ujumbe huo uweze kuendelea na majukumu kwa misingi ya mamlaka yake.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud