Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ISIL imekiuka Shari’ah, imekiuka sheria ya vita na kutenda uhalifu dhidi ya ubinadamu- Kamishna Zeid

UN Photo/Paulo Filgueiras
Kaminshna Mkuu wa haki za binadamu kwenye Umoja wa Mataifa Mwanamfalme Zeid Ra’ad Hussen. Picha:

ISIL imekiuka Shari’ah, imekiuka sheria ya vita na kutenda uhalifu dhidi ya ubinadamu- Kamishna Zeid

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu, Zeid Ra’ad Al Hussein, ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo kwamba, kundi linalotaka kuweka dola la Kiislamu lenye msimamo mkali, ISIL limetenda uhalifu uliokithiri nchini Iraq na kukiuka, siyo tu Shari’ah ya Uislamu, bali pia limekiuka sheria ya kimataifa, ikiwemo sheria ya kivita. Kamishna Zeid amesema hayo wakati Baraza la Usalama likikutana kuhusu hali nchini Iraq.

Kamishna Zeid, ambaye ameanza hotuba yake kwa kuorodhesha kila amri ya Uislamu ambayo ISIL imekiuka, amesema ulimwengu umeshangazwa na vitendo vya kinyama vya kundi hilo ambalo pia ameliita takfiri katika lugha ya Kiarabu, yaani watu wanaotaka kuwalazimishia wengine dhana zao za kidini.

Kwa kuzingatia ushahidi mkubwa uliopo sasa, hususan kuhusu Wayazidi, na ikisubiriwa uamuzi wa mahakama mwafaka ya sheria, huenda makosa matatu kati ya matano yaliyoorodheshwa chini ya Mkataba Kuhusu Mauaji ya Kimbari na Mkataba wa Roma, yametekelezwa na watu katika uongozi wa kitakfiri wa kundi lijulikanalo pia kama ISIL, ISIS au Da’ish. Kati ya makosa 11 yanayotambuliwa kama uhalifu dhidi ya ubinadamu katika Mkataba wa Roma, huenda wana hatia ya kutenda hadi makosa 9 miongoni mwayo. Kuhusu uhalifu wa kivita, bila shaka umetekelezwa katika makosa kadhaa katika muktadha husika.”

Kamishna Zeid amesema vitendo vya watu hao vinaghadhabisha mno, na kusema kuwa ukubwa wa unyama na ukatili wa ISIL dhidi ya raia unakiuka kila kanuni ya haki za binadamu.

Amesema dhana ya ISIL ya msimamo mkali imewezeshwa kuenea kufuatia miaka mingi ya migogoro nchini Iraq, akiongeza kuwa watu wa Iraq wamevumilia pia miaka ya ubaguzi, ufisadi, ukwepaji mkono wa sheria, na ukosefu wa kulinda haki zao za kiuchumi, kijamii, kiraia na kisiasa.