Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ripoti ya UNFPA kuhusu idadi ya watu yamulika umuhimu wa vijana bilioni 1.8

Vijana- picha ya @UNFPA

Ripoti ya UNFPA kuhusu idadi ya watu yamulika umuhimu wa vijana bilioni 1.8

Ripoti mpya ya mfuko wa idadi ya watu, UNFPA, imesema kuwa kuwapuuza vijana na kujali maslahi ya watu wazima pekee kunakwamisha chumi na jamii za ulimwengu kwa ujumla, ikisisitiza haja ya kujali hatma ya vijana ambao sasa idadi yao duniani ni bilioni 1.8. Taarifa kamili na Joseph Msami.

(Sauti ya Msami)

Ripoti hiyo ya kila mwaka inayoelezea hali ya watu duniani, imesema vijana wana umuhimu mkubwa kwani maamuzi kuhusu mustakhbali wa ulimwengu yanawahusu wao, na kwamba haki zao zinapaswa kulindwa.

Ripoti hiyo imesema, licha ya kuwepo ushahidi ya kwamba serikali zimeanza kuwajali vijana zaidi katika mikakati ya kisera, vijana bado wanakumbana na vizuizi vingi ambavyo huwazuia kuingia maisha ya utu uzima kwa hali salama na kupata ajira, kwani makumi ya mamilioni ama bado hawaendi shule, au wanaokwenda shule hawatimizi hata vigezo vya chini zaidi vya kupata elimu.

Ripoti imesema ingawa vizuizi hivyo vinaonekana kuwa sugu, vinaweza kuepukika kwa kuwawezesha vijana kuweka misingi ya maisha yao, na kufanya ajenda ya maendeleo baada ya mwaka 2015 kuwa na umuhimu kwa vijana.

Allana Armitage ni Mkurugenzi wa UNFPA, Geneva.

(Sauti ya Armitage)

"Hakujawahi kuwa na vijana wengi kama sasa, na huenda hakutawahi kuwa na fursa kama hii kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamiii. Kwa hiyo, jinsi tunavyokidhi mahitaji na ndoto za vijana leo, na kuwawezesha kufurahia haki zao, kutaamua mustakhbali wetu wa pamoja.”

Hadi asilimia 60 ya vijana katika nchi zinazoendelea ama hawana ajira, au hawapo shuleni, au wana ajira zisizoweza kutegemewa.