Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchi zisizo na bandari zahitaji kusaidiwa- Ban

Katibu Mkuu Ban Ki-moon.Picha ya UM/NICA

Nchi zisizo na bandari zahitaji kusaidiwa- Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, ban Ki-moon, amesema kuwa wakati ulimwengu unapofanya mipango ya kukabiliana na changamoto za kimataifa, ni lazima uzingatie hali ya nchi zinazoendelea zisizo na bandari.

Bwana Ban amesema hayo wakati akifungua kongamano la pili la Umoja wa Mataifa kuhusu nchi zinazoendelea zisizo na bandari mjini Vienna, Austria, akiongeza kuwa wakati mpango huo mpya wa kusaidia nchi hizo unapoandaliwa, ni lazima changamoto za kimataifa zizingatiwe.

Mabadiliko ya tabianchi. Majanga makubwa. Midororo ya kiuchumi na kifedha. Yote haya yana athari kwa matarajio yenu. Kongamano hili litaweka barabara ya kufuata kwa ajili ya nchi zinazoendelea zisizo na bandari.”

Ban amesema nchi hizo zimekuwa zikiuza bidhaa nje kwa wingi zaidi, lakini gharama ya uchukuzi bado ni ghali, mapato yatokanayo na kuuza bidhaa nje bado ni haba, na bidhaa zinazoagizwa kutoka nje ni ghali.

Tunahitaji kuungana zaidi kikanda. Hili litaimarisha ushirikiano wa kibiashara. Litajenga jumuiya thabiti zaidi. Muungano wa kikanda unaweza kuzibadili nchi zisizo na bandari kuunganishwa na bandari.”