Teknolojia duni yadhoofisha uwezo wa ukuaji Afrika

1 Novemba 2014

Kuwa na uwezo duni kiteknolojia ni mojawapo ya matatizo makubwa katika jitihada za bara la Afrika kufikia maendeleo endelevu.

Hili limebainika wakati wa ufunguzi wa warsha ya kila mwaka kuhusu uchumi barani Afrika ambapo kauli mbiu ya mkutano ya mwaka huu uliofanyika mjini Addis Ababa, Ethiopia ni maarifa  na ubunifu kwa ajili ya mabadiliko barani Afrika.

Maudhui ya mwaka huu yanaambatana na Ajenda ya Umoja wa Afrika ya 2063, msimamo wa pamoja wa Afrika wa Ajenda ya Maendeleo ya baada ya  mwaka wa 2015 ambayo imetambua sayansi, teknolojia na uvumbuzi kama nguzo muhimu kwa maendeleo Afrika.

Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ambaye pia ni Katibu Mtendaji wa Tume ya Uchumi ya Afrika, Carlos Lopez amesisitiza kuwa kuna haja ya kujenga uwezo wa kubadilisha ukuaji uwe ukuaji ubora barani.

Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, Nkosazana Dlamini Zuma amesema, Afrika inahitaji ujuzi, teknolojia, maarifa na uvumbuzi ili kuhakikisha demokrasia na utawala ambao unaweza kutoa huduma bora kwa umma na kuwezesha upatikanaji wa huduma za msingi kama vile chakula na lishe, maji na usafi wa mazingira, makazi, afya na elimu.

Kwa upande wake, Kaimu Mwanauchumi Mkuu na Makamu wa Rais  wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, Steve Kayizzi - Mugerwa,  amesema kuwa mkusanyiko wa kutosha wa ujuzi , teknolojia na maarifa kwa uvumbuzi ni muhimu kwa mabadiliko ya Afrika.

 

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter