Ugonjwa wa Tauni waweza salia historia Magadagascar- Dkt. Tedros
Mkurugenzi Mkuu wa shirika la afya ulimwenguni, WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema mlipuko wa ugonjwa wa tauni nchini Madagascar unaweza kusalia historia iwapo mamlaka nchini humo zitakuwa na uwekezaji wa kimkakati.
Dkt. Tedros amesema hayo leo huko Antananarivo, ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake ya kwanza kabisa tangu ateuliwe kushika wadhifa huo mwaka jana.
Amesema uwekezaji huo wa kimkakati ni muhimu kwa kuzingatia kuwa ugonjwa wa Tauni ni suala la mtambuka linalogusa siyo tu sekta ya afya bali pia umaskini na utayari wa mifumo ya afya kukabiliana na mlipuko na kuzingatia kanuni za kimataifa.
Dkt. Tedros ameshukuru hata hivyo mamlaka za Madagascar na wadau wa kimataifa kwa hatua walizochukua wakati wa mlipuko wa mwaka jana ambapo watu zaidi ya 200 walifariki dunia katika kipidi cha miezi minne.
Akizungumzia ziara hiyo, mwakilishi wa WHO nchini Madagascar, Charlotte Ndiaye amesema lengo ni kuimarisha hatua za kimtambuka zinazoenda pamoja na udhibiti wa wadudu wanaoneza ugonjwa huo wakiwemo panya bila kusahau ushiriki wa dhati wa serikali akisema..
(Sauti ya Charlotte Ndiaye)
“Tunadhani kwa azma ya kisiasa na utashi wa kisiasa tunadhani tunaweza kuzuia kabisa ugonjwa wa tauni Madagascar.”
Wakati wa ziara hiyo huko Madagascar, Mkuu huyo wa WHO atakutana pia na manusura wa ugonjwa wa tauni pamoa na familia zao.