Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa waonya unyanyapaa dhidi ya wahudumu wa afya

Dkt. David Nabarro akizungumza na waandishi wa habari. (Picha: Eskinder Debebe)

Umoja wa Mataifa waonya unyanyapaa dhidi ya wahudumu wa afya

Mratibu mwandamizi wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa kuhusu Ebola Dk David Nabarro ameelezea kusikitishwa kwake na kile alichokiita vizuizi na uwekwaji karantini kwa wahudumu wa afya wanaotoka kutoa huduma dhidi ya ugonjwa huo.

Akiongea na waandishi wa habari mjini New York Dk Nabarro amesema kumekuwepo na kutendewa visivyo kwa wale wanaorejea katika nchi zao wakitokea kwenye maeneo yalioathirika.

(SAUTI DK NABARRO)

Hakuna msingi wa kisayansi kwa vikwazo vya kusafiri na uwekwaji karatini kwa wahudumu wa afya ambao hawana dalili za ugonjwa. Hili halipaswi kuendelea. Wahudumu wa afya ni watu maalum ambao wanajitolea kibinadamu. Wanaougua kwa huduma hiyo waungwe mkono na sio kunyanyapaliwa.

Kuhusu kuibuka kwa ugonjwa wa Ebola nchini Mali Dk Nabarro amesema UNMEER inaendelea an mikakati ya dharura na tayari imeshachukua hatua muhimu za maandalizi  ikiwemo mafunzo na kuboresha vifaa tiba.

Kwa mujibu wa shirika la Afya ulimwenguni WHO,  hadi Oktoba 27 mwaka huu zaidi ya visa 13,000 vimeripotiwa na  vifo takribani 5,000 huko Guinea, Sierra Leone na Liberia.