Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Visa vya Ebola vyazidi 13,700, vifo ni zaidi ya 4,500- WHO

Picha: UNICEF Sierra Leone/2014/Dunlop

Visa vya Ebola vyazidi 13,700, vifo ni zaidi ya 4,500- WHO

Shirika la Afya Duniani, WHO limesema leo kuwa idadi ya visa vya Ebola Afrika Magharibi sasa hivi imepanda na kufikia watu zaidi ya 13,700. Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi, Dkt. Bruce Aylward, Msaidizi wa Mkurugenzi Mkuu wa WHO anayehusika na operesheni za kukabiliana na mlipuko wa Ebola, amesema kuwa nchi tatu za Liberia, Guinea na Sierra Leone, ambazo zimeathiriwa zaidi na mlipuko wa Ebola, zinachangia visa 13,676 vya idadi nzima.

“Ni 6,535, Liberia, 5,235 Sierra Leone, na Guinea, 1,906. Vifo sasa ni zaidi ya 4,500. Hatujapata takwimu kamili kuhusu vifo sasa, na zitatolewa baadaye usiku.”

Kuhusu vifo kutokana na Ebola, Dkt. Aylward amesema

“Lililo muhimu kwangu kuhusu vifo, na hili tumelizungumzia, sio idadi ya vifo vinavyoripotiwa, mbali ni kiwango cha watu tunaojua wanafariki dunia kutokana na Ebola. Na tunajua bado kuwa, kiwango cha vifo kwa wagonjwa ambao tunaweza kufuatilia hadi mwisho, ni asilimia 70.”

Amezungumzia pia umuhimu wa kuwafikisha wagonjwa katika vituo vya matibabu, kama ushahidi wa awali unavyoonyesha

“Unaonyesha kuwa kuwafikisha watu kwenye vituo vya matibabu inawapa fursa ya kunusurika kifo. Wakati mwingine ni vigumu kujua hilo kupitia takwimu, kwa sababu ya matatizo ya takwimu kuonyesha hilo moja kwa moja, lakini ni dhahiri kuwa kuna fursa ya kunusurika kifo, iwapo watu wanafikishwa kwenye vituo vya matibabu na kusaidiwa kuwa na maji mwilini, na huduma nyingine za kuwasaidia

Dkt. Aylward amesema kuwa serikali ya Mali imejikita katika kuwafuatilia watu waliokuwa kwenye basi alililosafiria mtoto aliyegunduliwa kuwa na Ebola, akiwa amesafiri kutoka Guinea, akiongeza kuwa kufikia sasa watu 84 wametambuliwa.