Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ofisi ya Haki za Binadamu yasikitishwa na kuzuiliwa kwa mtetezi wa haki za binadam Bahrain

Rupert Colville

Ofisi ya Haki za Binadamu yasikitishwa na kuzuiliwa kwa mtetezi wa haki za binadam Bahrain

Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na Haki za Binadamu, imeelezea kusikitishwa na kuzuiliwa kwa mtetezi wa haki za binadamu nchini Bahrain, Nabeel Rajab, tangu Jumatano aliporejea kutoka ziara yake ng’ambo alikojadili kuhusu hali ya haki za binadamu nchini humo na watu kadhaa, ikiwemo Ofisi ya Haki za Binadamu mjini Geneva.

Rajab ameshutumiwa kutoa matusi kwa taasisi ya serikali hadharani kwenye mitandao ya kijamii, na kuzuiliwa hadi Alhamis wiki ijayo, uchunguzi unapoendelea.

Mwanaharakati huyo wa haki za binadamu alikuwa ameachiwa huru tu mwezi Mei, baada ya kumaliza kifungo cha miaka miwili kwa kilichotajwa kama kosa la kufanya mkutano kinyume na sheria, na kuudhi taasisi rasmi.

Ofisi ya Haki za Binadamu imetoa wito kwa mamlaka za Bahrain kumwachia huru mara moja Bwana Rajab, na wengine wote ambao wamefungwa kwa kufurahia haki zao kwa amani. Rupert Colville ni msemaji wa Ofisi ya Haki za Binadamu, Geneva

“Kuwazuilia watetezi mashuhuri wa haki za binadamu kama Nabeel Rajab na Maryam Al-Kwaja kunapeleka ujumbe wa kutisha kwa wanaharakati ambao hawajulikani kuhusu hatma yao iwapo wataikosoa serikali kwa njia yoyote. Watetezi wa haki za binadamu nchini Bahrain ni lazima waweze kufanya kazi yao bila kuogopa kuadhibiwa.”