Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

CERF yatoa dola Milioni 3.8 kukabiliana na Ebola

Mkuu wa OCHA, Bi. Valerie Amos (Picha ya UM)

CERF yatoa dola Milioni 3.8 kukabiliana na Ebola

Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na misaada ya dharura ya kibinadamu, OCHA, Valerie Amos amesema ametenga dola Milioni Tatu Nukta Nane kutoka mfumo wa dharura wa majanga, CERF kwa ajili ya kusaidia operesheni za anga za kukabialiana na mlipuko wa Ebola huko Afrika Magharibi.

Taarifa ya OCHA imesema kupungua kwa safari za ndege kwenye ukanda huo umekwamisha harakati za kupeleka wahudumu wa afya na vifaa tiba na hivyo kuathiri mipango ya kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa huo.

Bi. Amos amesema fedha hizo zitasaidia operesheni hiyo inayoendeshwa na shirika la mpango wa chakula duniani, WFP linalosaidia kusafirisha watendaji, vifaa tiba na shehena nyingine muhimu zinazotakiwa kwenye maeneo yaliyo ndani zaidi huko Guinea, Liberia, Nigeria na Sierra Leone.

Akizungumzia usaidizi huo, Mratibu mwandamizi wa Umoja wa Mataifa kuhusiana na mlipuko wa Ebola Dokta, David Nabbaro amesema utawezesha watendaji wa Umoja huo na mashirika mengine kufika maeneo husika haraka iwezekanavyo.

Hadi leo wadau wa kibinadamu wamepokea dola Milioni 7.6 kutoka CERF.