Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban akaribisha makubaliano ya kusitisha mapigano Ukraine

Katibu Mkuu Ban Ki-moon. Picha@UM

Ban akaribisha makubaliano ya kusitisha mapigano Ukraine

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amekaribisha habari za kutia moyo kwamba mazungumzo ya leo baina ya kundi la wapatanishi na wawakilishi wa makundi yaliyojihami yamesababisha makubaliano ya usitishaji mapigano nchini Ukraine.

Ban amekaribisha mazungumzo ya hivi karibuni kati ya marais wa Ukraine na Urusi, akisema kuwa yamechangia hatua ya leo ya ufanisi, huku akihimiza mazungumzo hayo yaendelee.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephen Dujarric amewaambia waandishi wa habari kuwa Ban amesisitiza uangalizi wa kuaminika na wa kina pamoja na kuhakiki vitu muhimu kwa ufanisi katika utekelezaji wa makubaliano hayo ya kusitisha mapigano pamoja na mpango wa amani.

(Sauti ya Dujarric)

“Amehamasisha wote ambao wameridhia makubaliano hayo kuonyesha nia njema na kuchukua hatua madhubuti ili kutekeleza haraka iwezekanavyo na kwa ufanisi. Halikadhalika ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuunga mkono makubaliano hayo kwa maslahi ya amani endelevu kwa kuzingatia suluhu itakayojali utaifa na mamlaka ya Ukraine.”

Katibu Mkuu amerejelea wito wake kuwa hakuna suluhu la kijeshi kwenye mzozo wa Ukraine na ni vyema sasa kumaliza kabisa hali hiyo ili jamii ziweze kurejea kwenye maisha yao ya kawaida.