Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

OCHA yataja mambo matatu muhimu kwa Ukraine

Mkuu wa OCHA, Bi. Valerie Amos (Picha ya UM)

OCHA yataja mambo matatu muhimu kwa Ukraine

Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na misaada ya kibinadamu, OCHA, Valerie Amos, amezungumza huko Sloviansk, Ukraine mwishoni mwa ziara yake ya kujionea hali halisi na kutaja mambo matatu ya usaidizi ambayo ni muhimu ili kurejesha amani na utulivu nchini humo.

Mambo hayo ni pamoja na majadiliano ya kisiasa yanayoendelea ambayo Mkuu huyo wa OCHA amesema hitimisho lake litaleta amani, ulinzi na  usalama wa kudumu nchini Ukraine kwani kadri mzozo unavyoendelea athari zake zinaongozeka halikadhalika idadi ya watu wanaopoteza makazi.

Bi. Amos ametaja jambo la pili kuwa ni kusaidia jitihada za serikali ya Ukraine za operesheni za usaidizi wa kibinadamu ikiwemo kuongeza vifaa vinavyohitajika na kuangalia jinsi ya kufikia maeneo ambayo ni vigumu kufikika kwa sasa kwa kuzingatia .

Jambo la tatu ni ukarabati akisema kunahitajika jitihada za ukarabati zitakazochukua muda mrefu kwa kuzingatia uharibifu uliofanyika wa miundombinu muhimu.

Amesema Umoja wa Mataifa utaisaidia tathmini ya uharibifu na watafanya kazi kuhakikisha kuna wadau wa aina mbali mbali, nchi hisani na Benki ya dunia na wengineo ambao wanaweza kutoa misaada ya rasilimali kwa ajili ya jitihada hizo za muda mrefu

Mkuu huyo wa OCHA amesema Sloviansk, ni mfano wa vile ambavyo huduma za msingi zinaweza kurejeshwa kwa muda mfupi na tayari wananchi wanarejea kwenye makazi yao mjini na hivyo ni ishara ya umuhimu wa amani inayopaswa kuigwa kwenye miji mingine ya Ukraine ambako mapigano yanaendelea.