Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Oman yaridhia Mkataba wa kupiga marufuku matumizi ya mabomu ya ardhini

UN Photo/Robel Mockonenn
Bomu la ardhi likilipuliwa.

Oman yaridhia Mkataba wa kupiga marufuku matumizi ya mabomu ya ardhini

Oman imeridhia mkataba wa kimataifa wa Ottawa unaopinga matumizi, uzalishaji na biashara ya mabomu ya kutegwa ardhini na hivyo kufanya idadi ya nchi zilizotia saini mkataba huo kufikia 162.

Sherehe za utiaji saini mkataba huo zimefanyika leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, ambapo mwakilishi wa kudumu wa Oman, Balozi Lyutha Sultan Al-Mughairy amesema Oman imeridhika na kuungana na nchi nyingi duniani zilizojituma kupambana na matumizi ya mabomu hayo.

Amesema silaha hizo ambazo zinaua bila kuchagua hazina nafasi kwenye dunia ya leo, na kila nchi ina jukumu katika kusitisha mateso yanayosababishwa na silaha hizo.

Oman itaanza kutekeleza mkataba huo, tarehe mosi, Februari, 2015 ambapo hadi siku hiyo, Oman inatakiwa kuripoti kuhusu akiba yake ya mabomu ya ardhini.

Mkataba wa kupiga marufuku mabomu ya ardhini ulisainiwa Ottawa mwaka 1997, na ulianza kutekelezwa mwaka 1999. Tangu mwaka huo, zaidi ya mabomu milioni 47 yaliyowekwa akiba yamebomolewa.