Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO yataka mifumo ya kufuatilia magonjwa ya wanyama iimarishwe

World Bank/Curt Carnemark
Ngamia watuhumiwa hasa katika kueneza virusi MERS.

FAO yataka mifumo ya kufuatilia magonjwa ya wanyama iimarishwe

Wakati mkutano wa mawaziri wa afya na kilimo ukiendelea huko Indonesia, Shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO limesema mifumo ya ufuatiliaji wa magonjwa ya wanyama unahitaji usaidizi endelevu ili kuzuia vitisho kwa magonjwa ya binadamu. George Njogopa na taarifa kamili.

Taarifa ya George

Akizungumza kwenye ufunguzi wa mkutano wa kimataifa wa afya unaofanyika mjini Jakarta Afisa Mkuu wa wanyama Juan Lubroth alisema kuwa bado hakuna mkazo wa kutosha kushughulikia kitisho cha magonjwa yatokanayo na wanyama.

Alitolea mfano mlipuko wa ebola katika eneo la Afrika Magharibi kuwa ni kielelezo mojawapo ambacho kinafahamisha namna dunia ilivyoshindwa kutoa kipaumbele cha magonjwa hayo.

Alisema kuwa kuzuka kwa ugonjwa huo ni kama kengele kwa dunia kwamba inapaswa kuunga mkono mikakati inayohusu afya ya jamii hasa katika nchi zinazoendelea.

Alisema  kuwa wakati huu ambapo kunaongezwa msisitizo wa kukabiliana na kusambaa kwa ugonjwa, taarifa zinaonyesha kwamba  inadhaniwa kuwa tatizo hilo kwa mara ya kwanza liliipuka wakati virusi vya ugonjwa huo vilipotoka kwa wanyama wa mwituni na kwenda kwa binadamu.

Mkutano huo ambao unafikia tamati Agusti 21 pia unahudhuriwa na wataalamu wa magonjwa ya binadamu na wanyama .