Mchicha zao la kiasili kwa mwezi Agosti: FAO

11 Agosti 2014

Shirika la chakula na kilimo duniani, FAO limetangaza Mchicha kuwa ni zao la kiasili kwa mwezi huu wa Agosti likisema kuwa lina virutubisho muhimu kwenye majani yake au mbegu. Taarifa kamili na Grace Kaneiya..

(Taarifa ya Grace)

Ukijulikana kwa jina la kitaalamu Amaranthus au mchicha kwa lugha ya Kiswahili, FAO imesema unaweza kuliwa kama mboga ya majani au mbegu zake kutumika kuongeza ladha kwenye mchuzi wa nyama au kwenye uokaji wa mikate na kwenye chokoleti.

FAO imesema mchicha unafaa kwa wagonjwa wa Moyo, tumbo na wale wenye upungufu wa damu.

Ingawa imesema zao hilo hulimwa kwenye maeneo machache bado linafaa kuwa zao la biashara kwa soko la ndani na hata soko la nje.

Kwa mujibu wa FAO asili ya mchicha ni Amerika ya Kusini kwenye eneo la Andean ikiwemo Argentina, Peru na Bolivia lakini majani yake yanatumiwa zaidi kama mboga barani Afrika, Caribbean, India na China.

FAO ilianzisha zao la asili kwa kila mwezi ili kuibua mazao ya kiasili ambayo sasa yamesahaulika lakini iwapo yatatumika yanaweza siyo tu kuinua kipato cha wakazi wa eneo husika bali pia kuboresha afya zao.