Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwakilishi wa UM akaribisha nia ya kuundwa utawala mpya kati mwa Somalia

Nicholas Kay, Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia. Picha@UNSOM

Mwakilishi wa UM akaribisha nia ya kuundwa utawala mpya kati mwa Somalia

Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia Nicholas Kay, amekaribisha makubaliano na nia ya kuunda utawala katika eno la Kati nchini Somalia.

Viongozi wa eno hilo walitia saini makubaliano yanayolenga kutekeleza mpango wa kuunda utawala kati mwa Somalia, wakiongozwa na serikali kuu ya Somalia. Makubaliano hayo yalishuhudiwa na mabalozi wa nchi kadhaa na wawakilishi wa ngazi za juu wa nchi za Muungano wa Afrika, IGAD, Muungano wa nchi za Ulaya, EU, na Umoja wa Mataifa.

Bwana Kay amesema licha ya kwamba huu ni mwanzo tu wa kuunda utawala wa kitaifa kati mwa Somalia, ni ishara kuwa nchi hiyo inaendela kukaribia kufikia malengo ya mtazamo wa mwaka 2016 pamoja na kuundwa kwa katiba ya muda ya serikali kuu.

Bwana Kay amesema kuwa harakati za kuunda serikali ya majimbo zinalenga kuimarisha na kuleta amani nchini Somalia. Hata hivyo, ameongeza kusema kuwa kujenga utawala jumuishi katika eneo hilo la kati nchini Somalia kutakuwa na matatizo ya hapa na pale, lakini yote yanaweza kutatuliwa panapo maelewano baina ya pande zote husika.

Amehimiza pande hizo kushirikisha wanawake katika mipango na kuundwa kwa utawala wa mikoa ili kulinda mahitaji ya utawala wa sasa na ujao.

Amesema kuwa Umoja wa Mataifa utaendelea kusaidia serikali kuu ya Somalia katika juhudi za kujenga amani ya kudumu nchini humo