Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Magereza yafunguliwa kwenye kambi za UNMISS

Wanawake wakiteka maji kwenye kambi ya Bor, UNMISS. Picha@UNMISS

Magereza yafunguliwa kwenye kambi za UNMISS

Visa vya uhalifu kwenye kambi za wakimbizi wa ndani Sudan Kusini vimepelekea kufunguliwa kwa magereza kwenye kambi hizo kwa ajili ya kuwafunga waliotekeleza uhalifu.

Taarifa zaidi na Amina Hassan

Kwa ujumla, magereza manne yamejengwa katika kambi za Bor, Bentiu, Juba na Malakal, na tayari yamepokea zaidi ya watu 300, chini ya ulinzi wa polisi wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini SudanKusini, UNMISS.

Lengo la magereza hayo ni kufunga kwa muda walioshukiwa kutenda vitendo vya uhalifu, kabla ya kuwakabidhi kwa mamlaka za serikali, ikiwa hakuna hatari kwao kutoka nje ya kambi, jinsi anavyoeleza msemaji wa UNMISS, Joe Contreras akiongea na mtangazaji wa Redio ya UNMISS, Miraya FM. .

“ Kuna kamati za utathmini wa hatari za ukabidhi, ambazo zinapitia visa vyote vya watu binafsi ambao wamefungwa kwenye magereza hayo baada ya kushutumiwa kwa kitendo cha uhalifu. Hizo kamati zinashirikisha wafanyakazi wa UNMISS pamoja na viongozi wa jamii ya wakimbizi hawa wa ndani. Wanaamua pamoja kama ni sawa kuwakabidhi kwa mamlaka za serikali.”   

Mpaka sasa hivi, kesi 11 zimepelekwa kwa mamlaka za serikali. Contreras ameongeza, visa vya uhalifu vinavyoshuhudiwa kambini ni pamoja na kupigana, kutumia au kuuza madawa ya kulevya, na kubaka.