Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sheria zinazolinda watu zinaweza kusaidia kutokomeza Ukimwi

Picha@UNAIDS

Sheria zinazolinda watu zinaweza kusaidia kutokomeza Ukimwi

Kongamano la kimataifa kuhusu Ukimwi ambalo limekuwa likiendea mjini Melbourne, Australia, limehitimishwa kwa wito kwa serikali zipitishe sheria zinazowalinda watu badala ya zile zinazowakandamiza na kuwafanya wasijitokeze kupima na kutafuta huduma za matibabu dhidi ya virusi vya HIV.

Washiriki kwenye  kongamano hilo wamehitimisha kuwa inawezekana kutokomeza Ukimwi, lakini mapambano hayo yanapaswa kuzingatia suala la sheria na haki za binadamu, hususan za makundi ya jamii yaliyo hatarini zaidi.

Madeep Dahliwal, Mkurugenzi wa idara ya ukimwi katika Shirika la Umoja wa mataifa katika mpango wa maendeleo  ameeleza jinsi sheria mwafaka zinaweza kuchangia kukabiliana na Ukimwi.

"Kwa mfano, tunatumia mabilioni ya dola juu ya kuzuia maambukizi na juu ya huduma za matibabu na kwa upande mwingine kuna sheria na utekelezaji wa sheria ambao kwa kweli unasababisha watu kujificha na kukwepa huduma. Kwa kweli kama kuna vyombo vya sheria ambavyo ni vya kikatili na unaadhibu watu badala ya kuwasaidia kupata huduma za afya, huwezi kweli kupata faida kutokana na dola ulizowekeza katika kupambana na UKIMWI"

Washiriki wamemulika mchango wa watunga sheria na watunga sera katika kuhakikisha kuwa kuna mikakati ifaayo ya sheria inayotokana na ushahidi na haki za binadamu, badala ya zile zinazotokana na hofu na ubaguzi.