Fao yahitaji msaada wa dharura kukabili baa la njaa SAHEL.

Fao yahitaji msaada wa dharura kukabili baa la njaa SAHEL.

Umoja wa mataifa leo kupitia Shirika la chakula duniani FAO, umetoa wito kwa nchi wanachama kuangazia upya makubaliano ya hapo awali ya kupambana na  baa la njaa na uhaba wa chakula ili kulinda na kuongeza juhudi za kuboresha maisha ya  jamii maskini katika ukanda wa  SAHEL.

Taarifa kamili na John Ronoh

Kumekuwa na matatizo kadhaa yanayochangia uhaba wa chakula, yakiwemo yale yanayosababishwa na mapigano na ukame wa kila mara ambayo yameendelea kuzorotesha usalama wa chakula katika eneo hilo.

Msemaji wa FAO mjini Roma, Italia Domique Burgeon ameleeza kuwa katika mwezi wa pili mwaka 2014, FAO iliweka mkakati wa miaka mitatu kuhusu SAHEL ili kusaidia waathiriwa zaidi ya milioni 20 ambao wamekabiliwa na baa la njaa.

"Kwa bahati mbaya, Sahel haijazingatiwa sana na Sahel imeathirika na tatizo la aina ya kudumu na ambalo halisikiki sana, hasa kama ukiangalia mazingira magumu na utapiamlo uliokithiri ambao ni miongoni mwa viwango vya juu zaidi duniani. Katika eneo la Sahel msaada unaohitajika zaidi na kwa haraka ni fedha ili kujenga uhimili na jamii bora".

Bwana Burgeon amesema kwamba, kufukia sasa, msaada ambao umetolewa ni kiasi cha asilimia 28 ya msaada unaohitajika. Ameongeza kusema kuwa kuna haja ya kuongeza juhudi za kutoa ufadhili zaidi ili kuwezesha FAO kuokoa maisha ya waathiriwa kwa sababu ya utapiamlo iliokithiri katika eneo la Sahel.