Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNRWA yalaani mashambulizi kwenye shule yake

Watoto kutoka Yarmouk. UNRWA/Rami Al-Sayyed

UNRWA yalaani mashambulizi kwenye shule yake

Wakati huo huo, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Palestina, UNRWA, limelaani vikali kurushwa kwa makombora kwenye shule yake, Gaza katikati.

Taarifa zaidi na John Ronoh.

Zaidi ya watu 300 waliolazimika kuhama makwao kutokana na mashambulizi ya hivi karibuni walikuwa wametafuta hifadhi katika shule hiyo ya UNRWA. Makombora yaliyopiga shule hiyo mapema leo na jana na kujeruhi mtu mmoja yanadaiwa kurushwa na jeshi la Israel.

Mkurugenzi wa UNRWA, Pierre Krahenbuhl, amesema kwamba UNRWA iliiarifu awali Israel kwamba shule hiyo ilikuwa ni hifadhi wa wakimbizi. Ameiomba serikali ya Israel ifanye utafiti juu ya mashambulizi haya ya majengo ya Umoja wa Mataifa, ambayo yanahatarisha maisha ya wakimbizi na wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa.

Halikadhalika, Naibu Katibu Mkuu wa Maswala ya Kibinadamu, Kyung wha Kang, ameonya kwamba hali ya kibinadamu inazidi kuwa mbaya katika ukanda wa Gaza, wapalestina 600 wakiwa wameshafariki dunia, na waisraeli 28, wakiwemo wajeshi 26.

Amesema, theluthi moja ya vifo vya wapalestina ni watoto, akieleza kwamba raia hawajui pa kukimbilia. Wengine, amesema, wameamua kutawanyika na familia zao kwenye maeneo tofauti, ili wasiwe katika hatari ya kufa wote kwa wakati mmoja, hii ikiwa ni dalili ya kuwa kwenye hali ya kukata tamaa kabisa.