Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sitisha mapigano kwanza Gaza kuokoa maisha ya wananchi: UNOCHA

Mkaazi wa Palestina akipita mbele ya askari wa Israeli mashariki mwa Jerusalem. Picha: IRIN/Andreas Hackl(UN News Centre)

Sitisha mapigano kwanza Gaza kuokoa maisha ya wananchi: UNOCHA

Mratibu wa masuala ya kibinadamu katika Umoja wa Mataifa, OCHA, James Rawley, amesema kwamba amesikitishwa na mapigano ya wiki hii ambayo yamewaathiri zaidi wananchi wa kawaida wa Ukanda wa Gaza. Rawley amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari alipotembelea shule iliyopigwa bomu kwenye ukanda huo, akiandamana na Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuwasaidia Wakimbizi wa Palestina, UNRWA, Pierre Krähenbühl, ambaye amesema:

“ Tunawawazia wananchi ambao tayari wamefariki dunia, na wengine wengi zaidi ambao wamejeruhiwa kimwili ama kisaikolojia. Wasiwasi wetu wa kwanza ni usalama  wa wananchi popote walipo. Ndiyo maana ombi letu la kwanza ni kurejesha utulivu na kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano ili kuzuia vifo vingine ambavyo havihitajiki”

Amesisitiza umuhimu kwa pande zote kuheshimu sheria za kimataifa za kibinadamu, ikiwemo kujizuia kushambulia raia au mali zao, akiongeza:

“ Leo tumeona uharibifu uliotokea mpaka sasa hivi na madhara ya kibinadamu yanayoibuka, ikiwemo kuharibika kwa shule 66 na nyumba zaidi ya 940, pamoja na miundombinu ya afya, maji, usafi, elimu na umeme. Huu hasa unaongeza ugumu wa kutoa huduma za msingi. Juu ya hayo, takriban Wapalestina 16,000 wameshakimbia makwao na kutafuta hifadhi katika sehemu kama hii tuliyopo leo”

Amesema, anawawazia hasa watoto wa Gaza, ambao hofu yao na ukosefu wa usalama zitasababisha kovu ambalo litabaki daima.  Ingawa lengo la kwanza ni kusitisha mapigano, amesema ni lazima kukabilinana na mizizi ya mzozo unaokumba Gaza, iwe kwa upande wa siasa au usalama, lakini pia wa maendeleo ya ukanda huo, akitaja shida watu wa Gaza wanazokumbana nazo katika kusafiri, na kupata umeme na maji.