Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF yawasikitikia watoto wanaoathirika na mapigano Gaza

UN Photo/Shareef Sarhan
Watoto wawili wakisimama mbele ya nyumba ambayo polisi imesema imepigwa bomu la anga na Israel kwenye kambi la wakimbizi la Maghazi katikati mwa Ukanda wa Gaza.

UNICEF yawasikitikia watoto wanaoathirika na mapigano Gaza

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na watoto UNICEF Anthony Lake amesema mapigano yanayoendelea huko Gaza yamegeuza maisha ya watoto kua magumu huku kiasi cha 33 wakiwa wamepoteza maisha katika siku za hivi karibuni kutokana na mapigano hayo. Taarifa kamili na George Njogopa

Taarifa ya George

Mkurugenzi huyo ambaye amesisitiza kuwa hakuna sababu kwa watoto hao kuumia kutokana na machafuko hayo amesema kuwa hali ya wasiwasi inaendelea kuongezeka na kwamba watoto wengi wanaumizwa kimwili na kisaikolojia.

Amesema kuwa mara nyingi uzoefu unaonyesha kwamba watoto wanaoshuhudia mara kwa mara mapigano ya namna hiyo hujenga tabia ya kuyatizama kama ni matukio ya kawaida na hivyo wanaweza kuyarudia kwenye maisha yao ya baadaye.

Katika hatua nyingine maofisa wa UNICEF wametembelea eneo la mapigano na kuzungumza na familia ambazo zimesimulia maisha ya magumu wanayokumbana nayo.

Familia hizo zilisema kuwa kuna hali ya dhiki na kutisha inayowaandama watoto wengi ambao baadhi yao wanakosa usingizi nyakati za usiku kutokana na kuingiwa na woga.