Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Biashara haramu ya viumbe wa pori hufadhili makundi ya uhalifu kutishia usalama: UNEP

Ndovu (picha ya UNEP)

Biashara haramu ya viumbe wa pori hufadhili makundi ya uhalifu kutishia usalama: UNEP

Ripoti mpya iliyotolewa leo na Shirika la Mpango wa Maendeleo, UNEP,  na polisi ya kimataifa, INTERPOl, imesema kuwa biashara haramu inayohusu mazingira, ambayo ina thamani ya hadi dola bilioni 213 kila mwaka, inasaidia kufadhili makundi ya uhalifu, makundi yanayojihami na yale ya kigaidi, na hivyo kuhatarisha usalama na maendeleo endelevu ya mataifa mengi.

Ripoti hiyo iliyopewa kichwa, ‘Janga la uhalifu wa kimazingira, na ambayo imetolewa wakati wa Baraza la Mazingira mjini Nairobi, Kenya, imesema makundi ya kigaidi yanayoendeleza shughuli zao Afrika ya Mashariki yanakadiriwa kupata kati ya dola milioni 38 na milioni 56 kila mwaka kutokana na biashara haramu ya mkaa.

Ripoti imeongeza kuwa kwa ujumla, makundi yenye silaha na yale ya kigaidi katika nchi za Afrika zenye migogoro inayoendelea yanaweza kupata kati ya dola milioni 111 na 289 kila mwaka kutokana na kuhusika kwao katika biashara haramu ya mkaa, au kwa kutoza ushuru biashara hiyo. Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric amewadokezea waandishi wa habari kuhusu ripoti hiyo…

Sauti ya Dujarric

“Biashara kama hii haramu katika rasilmali za asili inatishia usalama na maendeleo endelevu ya mataifa mengi. Kwa kulinganisha, thamani nzima ya faida inayotokana na uhalifu wa kimataifa wa mazingira, inazidi kiasi cha fedha zinazotolewa kwa usaidizi wa maendeleo ya kimataifa ambazo ni takriban dola bilioni 135 kila mwaka.”

Takwimu za pamoja za Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na madawa na uhalifu, UNODC, Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo, OECD, UNEP na INTERPOL, zinaonyesha kuwa thamani inayotokana na uhalifu wa kimazingira, ambao unajumuisha ukataji misitu, ujangili na biashara haramu ya wanyama wa pori, uvuvi haramu, uchimbaji migodi haramu na kutupa taka za sumu, ni kati ya dola bilioni 70 na 213 kila mwaka.