Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukosefu wa ajira kwa vijana ni janga linalotokota: Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akikutana na vijana, @ILO

Ukosefu wa ajira kwa vijana ni janga linalotokota: Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amezungumza kwenye mjadala shirikishi ulioandaliwa na Shirika la kazi duniani, ILO huko Geneva kuhusu ajira kwa vijana akisema kuwa ukosefu wa ajira miongoni mwa kundi

(Taarifa ya Priscilla)

Kuwekeza kwa vijana ilikuwa moja ya mada ya mkutano huo ambapo Ban amesema dunia inakabiliwa na janga la ukosefu wa ajira miongoni mwao kwani nusu ya vijana duniani ni waajiriwa maskini au hawana ajira kabisa, akisema hilo ni jaribio kubwa zaidi kwa zama hizi.

Ametaja vijana wa kike kuwa wako hatarini zaidi wakifanya ajira zisizo na staha wakati huu ambapo ILO inatambua kuwa ajira siyo tu chanzo cha ujira bali pia ni suala la utu na staha, hivyo akasema..

“Kwanza ujumbe wangu kwa serikali, nasema wekezeni zaidi kwa mipango ya ajira kwa vijana, endelezeni ajira zenye staha. Sera za ajira kwa vijana ni msingi wa kuvuna mafanikio ya uwekezaji wenu wa kila siku kwenye elimu na mafunzo ya ufundi stadi.”

Ban amehoji ni ujumbe gani ambao dunia inatuma kwa vijana iwapo kundi hilo halitaona matumaini huku viongozi wakishangaa hatua za vijana kuonyesha kukata tamaa na kutoridhika.

Amesema mustakhbali unaotakiwa ni ule wenye vijana walio na ajira zenye staha na utu.

Kwa mujibu wa ILO zaidi ya vijana Milioni 74 duniani kote hawana ajira na wengine Milioni 228 ni wafanyakazi maskini.